Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Jawad Mervi, mjumbe wa Baraza Kuu la Hawza, mwishoni mwa darsa yake ya Khariji ya Fiqhi, alizungumzia ushindi mkubwa wa hivi karibuni wa Mujahidina wa Ansarullah wa Yemen katika Mlango wa kimkakati wa Bab al-Mandab, na kuutaja kuwa ni “Ushindi juu ya Ushindi”.
Jambo la kwanza: Kuwapongeza wananchi waliodhulumiwa na wanaopinga dhuluma nchini Yemen kwa “Ushindi juu ya Ushindi” wa hivi karibuni
Tunawapongeza wananchi waliodhulumiwa na wenye mwelekeo wa Wilaya nchini Yemen kwa “Ushindi juu ya Ushindi”. Nina taarifa kutoka ndani ya Yemen ambazo huenda hazijawafikia baadhi ya watu, taarifa ambazo ni zaidi ya yale yaliyotajwa katika mikusanyiko ya hadhara; lakini kwa kweli ulikuwa ni “Ushindi juu ya Ushindi”, kwa miaka 12, watu wa Bani Umayyah na Bani Marwan pamoja na watoto wao wamekuwa wakiwazingira wananchi hawa waliodhulumiwa, ni mzingiro mzito kiasi gani ambapo ni funzo kwa mataifa yote duniani, wananchi hawa walisimama imara na wakapinga dhuluma.
Ninawaelekezea maneno yangu Waislamu wa Ahlus-Sunna wenye uadilifu duniani kote: Wananchi hawa waliodhulumiwa, waliposimama kwa ajili ya suala la Palestina na Gaza, waliweka kila walichokuwa nacho na wakaonesha mshikamano na Ghaza na Palestina kwa kauli na kwa vitendo, lakini watoto wa Bani Umayyah na Bani Marwan miongoni mwa Ahlus-Sunna waliwafanyia nini wananchi hawa? Hata hivyo, ndani ya muda wa saa 12 walivunja kabisa mipango yao, na katika siku zijazo itafahamika waziwazi yale waliyoyafanya.
Tunawapongeza wananchi waliodhulumiwa na wanaopinga dhuluma nchini Yemen kwa ushindi huu mkubwa.
Pamoja na kwamba katika siku hizi chache zilizopita, uratibu kati ya Uturuki na Saudi Arabia uliwaingiza nchini Yemen maelfu kadhaa ya wanajeshi wa Takfiri kutoka Istanbul nchini Uturuki na Saudi Arabia, na walipoona kwamba wananchi hao wanataka kuvunja mzingiro, waliwaweka Waumayyah hawa dhidi ya wafuasi wa Amir al-Muuminina (a.s.), lakini wananchi wa Yemen wamepata ushindi gani mkubwa! Hili litadhihirika wazi katika siku zijazo.
Jambo la pili: Kulaaniwa shambulio la Taliban dhidi ya Chuo cha Khatam al-Nabiyyin (s.a.w.w.) nchini Afghanistan
Serikali ya Taliban nchini Afghanistan, ikiwa na fikra maalumu na mtazamo maalumu kuhusu Uislamu, kwa masikitiko makubwa tangu mwanzo wa harakati zake ilianza kuchukua hatua zisizofaa na zisizo na mantiki. Iliwanyima nusu ya idadi ya watu wa nchi hii, ambao ni wanawake, fursa ya elimu na masuala ya kijamii. Kisha ilianza kuchukua hatua dhidi ya wafuasi wa madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s.), ikawanyima haki zao, ikafunga Husainiya na kumbi, na leo imekishambulia Chuo kikubwa sana cha Kiislamu cha Kabul, Chuo cha Khatam al-Nabiyyin (s.a.w.w.), ikawakamata vijana wanafunzi wa elimu za kidini, na imeripotiwa kwamba iliwapiga na kuwadhulumu, huku baadhi ya walimu ikiwa imewachukua.
Ninawaambia Mullah wa Taliban: Ikiwa mna elimu, jifunzeni wenyewe; na ikiwa hamna elimu, mwambieni mtu awasomee historia ya Afghanistan, ili mjue kwamba wafuasi wa Ahlul-Bayt (a.s.) katika nchi hii wamekuwa sababu ya kubaki kwa nchi hii na kutogawanyika kwake. Walikuwa tayari kutoa maisha yao kwa ajili ya Afghanistan, na ndio waliokuwa sababu ya kuhakikisha usalama wa taifa katika nchi hii, waliifikisha katika kiwango cha juu kabisa roho ya udugu na upendo kati yao na ndugu zao Waislamu wa Ahlus-Sunna.
Ninawaambia: Isomeni historia yenu wenyewe, mjue namna mababu na wazee wenu walivyowatendea Mashia, ambao wana historia ya kuwepo huko tangu karne ya kwanza Hijria. Kila aina ya ukatili na mauaji ambayo mababu na wazee wenu waliitumia dhidi ya Mashia haikuweza kuwazuia wala kuwanyamazisha. Badala yake, wao wameendelea kustawi siku baada ya siku, na makundi yao yaliyoko Ulaya na Marekani leo yamekuwa wabeba bendera wa madhehebu yao.
Ninawaambia: Acheni kufanya mambo haya, mababu zenu hawakuweza kufanya lolote, nanyi pia acheni, kwa sababu hamtaweza kufanya lolote. Wanazuoni na viongozi wakuu wa Hawza wanafuatilia kwa karibu mienendo yenu, na itakapofikia wakati muafaka watachukua hatua inayofaa dhidi yenu.
Maoni yako